Chama Cha Mapinduzi, Idara ya Usalama wa Taifa na mkataba wa bandari
Moja ya kuu zinazotolewa kuhusu sababu zilizopelekea kuingia mkataba wa bandari ni upigaji uliokuwa ukifanyika kwenye bandari ya Dar es Salaam. Unaweza kujiuliza “kama tatizo ni upigaji katika bandari ya Dar es Salaam, kwanini basi mkataba huo uhusishe bandari zote nchini Tanzania?”
Hutopata jibu kwa sababu kama hujasoma mkataba huo utaambiwa kuwa unahusu bandari saba tu, na ukijaribu kwenda mbele zaidi na kuhoji ni bandari zipi hizo saba, au kwanini bandari saba na sio zote, utaishia kuambiwa kuwa umelipwa fedha na wapinzani wa mkataba huo.
Kutegemea unaongea na nani, orodha ya “wapinzani wa mkataba wa bandari” ni ndefu. Juu kabisa kwenye orodha hii ni “usual suspects”, Chadema - na specifically Mheshimiwa Tundu Lissu.
Pia kuna wanaharakati mbalimbali hususan wanasheria waliojitoa mhanga kupigania haki za Watanzania, kama vile wanasheria wasomi Boniface Mwabukusi na Peter Madeleka. Kwa bahati mbaya, Madeleka yupo ndani muda huu baada ya serikali kuamua kufuta “plea bargain” kwa vile tu mwanasheria huyo alikuwa mstari wa mbele kupinga mkataba huo.
Kuna watu kama Profesa Issa Shivji, Profesa Anna Tibaijuka, Jaji Warioba, Mzee Butiku na wengineo ambao nao wanaonekana “wapinzani wenye maslahi binafsi.”
Pia kuna viongozi kadhaa wa dini, hususan wa madhehehu ya Kikristo ambao wao wanashutumiwa kuwa wanaupinga mkataba huo kwa sababu “Rais ni Muislamu”.
Lakini hata Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na Makamu Mwenyekiti wa CCM Abdulrahman Kinana hawajasalimika, kwani nao wametajwa kuwa miongoni mwa wapinzani wa mkataba huo, wakituhumiwa kuwa wananufaika na ukwepaji kodi uliosababisha serikali kuchukua uamuzi wa kuingia mkataba huo mpya.
Kwa wananchi wa kawaida wasio na wadhifa wowote, kauli yoyote dhidi ya mkataba au hata kuhoji kuhusu mkataba huo huliibua genge kubwa la “chawa” linaloongozwa na baadhi ya wanahabari pamoja na wasanii.
Makala hii inaonyesha nafasi ya chama tawala CCM na Idara ya Usalama wa Taifa katika sakata hilo, na kuangalia athari za mkataba huo na mjadala unaouzunguka, kwenye mustakabali wa umoja wa kitaifa.