Dear Mama @SuluhuSamia: Mtu Huyu Hana Nia Nzuri Nawe, Anataka Kukufarakanisha Na Baadhi Ya Watu Wanaokusapoti
Dear Mama Samia,
Heri ya mwaka mpya 2025. Na uwe na heri na mafanikio.
Jana nilikutwiti Mama, kuhusiana na video iliyochapishwa juzi na mtu anayeitwa Cyprian Musiba, ambaye alinitaja kuwa miongoni mwa watu wanaokutukana, sambamba na kushirikiana na raia wa kigeni kukuhujumu na kuhamasisha uvunjifu wa amani.
Dear Mama, huyu mtu hajaanza tabia hii leo. Februari 2018, alinitaja kuwa miongoni mwa “Watu Hatari” waliopanga kuipindua serikali ya marehemu John Magufuli.
Na kwa takriban miaka mitatu mfululizo, aliendelea kunichafua kwa nguvu kubwa kupitia magazeti yake ya Tanzanite na Sayari Yetu na chaneli yake ya YouTube.
Dear Mama, sitaki kutumia tukio hili kuwa kama fursa ya mimi “kujisafisha” kwako, kwa sababu sijawahi katika wakati wowote ule kufanya chochote kile dhidi yako, sio tu kwa sababu wewe Mama ni Mkuu wa nchi bali pia kwa sababu bado nina imani na matumaini katika uongozi wako.
Ikumbukwe kwamba mimi ndiye nilikuwa Mtanzania wa kwanza kutangaza kuhusu kifo cha marehemu Magufuli, sio kwa sababu iwe breking news bali kwa sababu kulikuwa na mipango miovu ya kukiuka katiba kukuzuwia Mama usiwe rais.
Kadhalika, mara baada ya kufanikiwa kukwamisha jaribio hilo la ukiukwaji wa katiba na wewe Mama kuapishwa, nilikuwa mmoja wa watu wachache maarufu kujitokeza hadharani kukemea matusi dhidi yako yaliyojificha kwenye kivuli cha uanaharakati.
Na pengine mwanao Abdul hajawahi kukufahamisha kwamba niliwahi kuwasiliana nae nilipopata taarifa kuhusu mpango dhalimu wa kukuchafua mtandaoni, mpango uliomhusisha mtu mmoja ambaye sasa anajitanabaisha kama mtetezi wako mtandaoni.
Japo Abdul, hakunijibu, lakini naamini ujumbe husika ulifika na pengine kupelekea kutofanikiwa kwa mpango huu.
Tofauti na anavyojaribu kujinasibu muda huu, huyo mtoa tuhuma amekuwa miongoni mwa watu wanaoneza propaganda kwamba kifo cha marehemu Magufuli kilikuwa sio mapenzi ya Mungu bali “kazi ya watu waliouwa wanaiwinda nafasi yake (marehemu).” Nina hakika vijana wako wa Idara ya Usalama wa Taifa wanaweza kukuthibitishia hilo.
Kadhalika, alichofanya Musiba ni mwendelezo tu wa genge fulani ambalo linaamini kwamba kwa vile sijawahi kukukosoa katika namna nilivyokuwa namkosoa marehemu Magufuli - kwa sababu zilizo wazi - basi labda “unaweza kunikumbuka”.
Lakini kubwa zaidi, katika mwaka huu wa uchaguzi, kuna hofu kwamba labda nikaombwa kushiriki kwenye kampeni zako, kama nilivyoombwa mwaka 2015 kushiriki kwenye kampeni za marehemu Magufuli. Kwahiyo kinachofanyika ni ku- “preempt” uwezekano huo.
Mwisho, Dear Mama, mara kadhaa nimetanabaisha kuwa miongoni mwa sababu zinazonifanya niendelee kukuunga mkono, licha ya wajibu wangu wa kiraia, ni heshima yangu kwa wanawake. Marehemu mama yangu (Mwenyezi Mungu amlaze mahali mema peponi) alinifundisha kuwa “kila mwanamke ni taswira ya mama yako”, na kwangu heshima kwa “mama zangu” ni kama “amri ya Mungu”, sio suala la mjadala bali la lazima.
Kadhalika, Dear Mama, binafsi nina deni kubwa la shukrani kwako. Japo haipendezi kumsema vibaya marehemu, lakini kulifanyika majaribio kadhaa ya kunidhuru wakati wa utawala wa marehemu Magufuli, lakini mara baada ya wewe kuingia madarakani, umefanikisha kukomesha hilo japo watendaji wasio watiifu kwako waliwahi kufanya jaribio moja lililofeli.
Licha ya hilo, hata kijarida hiki na vinginevyo ninavyoandika sasa vinasomwa nchini Tanzania kutokana na wewe Mama kuondoa zuio la TCRA dhidi ya vyombo mbalimbali vya habari rasmi na visivyo rasmi kama kijarida hiki. Japo kuna “wasio na shukrani” wanaoweza kusema “ah si ametekeleza tu wajibu wa kikatiba”, sie tuliolelewa na kufundwa kuhusu umuhimu wa kushukuru, tunafahamu bayana kuwa hili liliwezekana tu kutokana na utashi wako na wala sio wajibu wa kikatiba, kama ambavyo ruhusa yako kwenye mikutano na maandamano ya wapinzani ilivyotokana na utashi wako binafsi na sio shinikizo lakikatiba/kisheria.
Uniwie radhi kwa kukuchukulia muda wako adimu lakini nimeonelea ni vizuri kuweka rekodi sawia, na wala sio kwa kuhofia kwamba unaweza kuamini tuhuma za Musiba - mzushi mzoefu aliyewahi kuwazushia tuhuma nzito za uongo viongozi mbalimbali nchini.
Nimalizie kwa kukutakia tena heri ya mwaka mpya.
Jamhuri ya Muungano, Kazi iendelee 🙏