UJASUSI (espionage) ni nini? Na MAJASUSI (spies) wanafanya kazi gani hasa? [Sehemu ya Tano: Ujasusi kama nyenzo ya kidiplomasia]
Hii ni makala ya tano katika mlolongo mrefu wa makala mbalimbali zinazohusu taaluma ya intelijensia. Huenda baadhi ya makala hizi zikazaa vitabu huko mbeleni kama ambavyo makala kuhusu “Afisa Usalama wa Taifa ni Mtu Gani? Na Anafanya Nini?” zilivyopelekea kitabu bora kabisa chenye jina hilo.
Makala/Sehemu ya kwanza ilihusu maana ya neno UJASUSI. Ni vema ukasoma sehemu ya kwanza na ya pili kabla ya kusoma sehemu ya tatu.
Makala ya pili ilihusu historia ya ujasusi
Makala ya tatu ilihusu aina za ujasusi
Makala ya nne ilimalizia kilichosalia katika sehemu ya tatu kuhusu aina za ujasusi.
Hata hivyo, kabla ya kuingia kwa undani, ni vema kujikumbusha kuwa mpangilio wa mada zinazounda mfululizo wa makala hizi, ambao ni kama ifuatavyo
ambao ni kama ifuatavyo:
👉Maana ya ujasusi
👉 Historia ya Ujasusi
👉 Aina za Ujasusi
👉 Ujasusi kama nyenzo ya diplomasia
👉 Tofauti kati ya Ujasusi na Uafisa Usalama wa Taifa
👉 Majasusi wanapatikanaje?
👉 Majasusi kazini
👉 Changamoto zinazoukabili ujasusi/majasusi duniani
👉 Changamoto za ujasusi/majasusi Tanzania
👉 Mashirika maarufu ya ujasusi duniani na majasusi maarufu duniani.
Ujasusi kama nyenzo ya diplomasia
Kwa vile historia ya ujasusi ilishaelezwa katika makala zilizotangulia, makala hii itatupia jicho historia ya diplomasia pekee licha ya ukweli kwamba inazungumzia vitu vyote viwili, yaani ujasusi na diplomasia.
Diplomasia ni sanaa na sayansi ya kudumisha uhusiano wa amani kati ya mataifa, vikundi au watu binafsi. Mara nyingi, diplomasia inarejelea wawakilishi wa vikundi tofauti wanaojadili maswala kama vile migogoro, biashara, mazingira, teknolojia, au usalama.
Watu wanaofanya diplomasia wanaitwa wanadiplomasia. Wanadiplomasia wanajaribu kusaidia nchi yao wenyewe, kuhimiza ushirikiano kati ya mataifa, na kudumisha amani. Kundi la wanadiplomasia wanaowakilisha nchi moja inayoishi katika nchi nyingine huitwa ujumbe wa kidiplomasia.
Ujumbe wa kudumu wa kidiplomasia unaitwa ubalozi. Balozi ni mwanadiplomasia mkuu katika ubalozi. Ujumbe mkubwa wa kidiplomasia unaweza kuwa na uwakilishi kando na ubalozi mmoja. Maeneo mengine ya uwakilishi huitwa balozi.
Historia fupi ya Diplomasia
Uwezo wa kufanya shughuli za kidiplomasia ni moja wapo ya mambo muhimu ya serikali. Diplomasia imekuwa ikitekelezwa tangu zama za kale za madola-miji (city-states).
Hapo awali wanadiplomasia walitumwa tu kwa mazungumzo maalum, na wangerudi mara baada ya kilichowapeleka huko kukamilika. Kwa kawaida, wanadiplomasia wa enzi za kale walikuwa ndugu wa familia inayotawala, na hii ilisaidia kuwapa uhalali wa kuwakilisha familia au ukoo unaotawala.
Tofauti moja kubwa ilikuwa kwenye uhusiano kati ya Papa na Mfalme wa Byzantini. Mawakala wa Papa, walioitwa apocrisiarii, walikuwa wakaaji wa kudumu huko Constantinople. Baada ya karne ya 8, hata hivyo, migogoro kati ya Papa na Mfalme (kama vile mabishano ya Iconoclastic kuhusu matumizi ya sanamu za kidini katika Ufalme wa Byzantini) ilisababisha kuvunjika kwa mahusiano haya ya karibu.
Mara nyingi inaaminika kuwa diplomasia ya kisasa ina asili katika majimbo ya Italia ya Kaskazini katika zama za mwanzo za Mwamko (Renaissance).
Balozi za kwanza zilianzishwa katika karne ya 13. Mji wa Milan ilikuwa nafasi muhimu katika maendeleo hayo, hasa chini ya Francesco Sforza ambaye alianzisha balozi za kudumu katika majimbo mengine ya miji ya Kaskazini mwa Italia. Ilikuwa nchini Italia ambapo tamaduni nyingi za diplomasia ya kisasa zilianza, kama vile uwasilishaji wa sifa za balozi kwa mkuu wa nchi.
Shughuli za kidiplomasia katika uchanga wake hatimaye zilienea kutoka Italia hadi mataifa mengine ya Ulaya. Milan ilikuwa ya kwanza kutuma mwakilishi katika mahakama ya Ufaransa mwaka 1455. Milan hata hivyo ilikataa kuwakaribisha wawakilishi wa Ufaransa wakihofia ujasusi na uwezekano wa kuingilia masuala ya ndani.
Na tukio hili ni miongoni mwa matukio ya mwanzo yanayopigia mstari uhusiano katika ya diplomasia na ujasusi.
Kadri mataifa ya kigeni kama vile Ufaransa na Uhispania yalivyozidi kujihusisha na siasa za Italia ndivyo hitaji la kukubali wajumbe (mabalozi) lilivyozidi kutambuliwa.
Muda si mrefu mataifa yote makubwa ya Ulaya yalikuwa yakibadilishana wawakilishi. Hispania ilikuwa ya kwanza kutuma mwakilishi wa kudumu ilipomteua balozi katika Mahakama ya Uingereza mwaka wa 1487. Kufikia mwishoni mwa karne ya 16, balozi za kudumu zikawa ni kama utaratibu wa kawaida.
Mikataba mingi ya diplomasia ya kisasa ilitengenezwa katika kipindi hiki. Cheo cha juu cha wawakilishi kilikuwa balozi. Balozi kwa wakati huu karibu kila mara alikuwa mtu mtukufu - cheo cha mtukufu kilitofautiana na heshima ya nchi aliyotumwa.
Kanuni za hadhi kwa mabalozi nazo ziliibuka, kwa mfano kuwa na makazi katika eneo kubwa, kuandaa karamu za kifahari, na kuhudhuria matukio muhimu ya taifa mwenyeji.
Huko Roma, balozi za Kikatoliki, Ufaransa na Uhispania wakati mwingine zilijumuisha misafara wa hadi watu mia. Kwa ujumla uendeshaji wa balozi ulikuwa na gharama kubwa.
Hadhi za mabalozi kutoka nje zilipangwa kwa kanuni ambazo mara nyingi zilibishaniwa sana. Kwa Roma, mabalozi kutoka Vatikani walikuwawa daraja la kwanza, kisha wale kutoka kwa falme, kisha wale wa umwinyi (duchies) na himaya za wana ufalme (principals). Wawakilishi kutoka jamhuri (republic) walichukuliwa kuwa wajumbe wa hadi ya chini kabisa.
Hata hivyo, kwa sababu mabalozi wakati huo walikuwa waheshimiwa wasio na uzoefu na diplomasia, walihitaji kuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi wa ubalozi. Wafanyakazi hao walikuwa wtaalamu wa sekta mbalimbali ambao walitumwa kwenye majukumu mbalimbali. Kadhalika, walikuwa na uelewa kuhusu nchi mwenyeji.
Baadhi ya wafanyakazi hawa walikuwa majasusi. Na hii inaonyesha tena uhusiano kati ya diplomasia na ujasusi.
Uhitaji wa watu wenye ujuzi wa kuwawezesha kufanya kazi kwenye ulipelekea ongezeko la masomo ya sheria za kimataifa, lugha za kisasa, na historia katika vyuo vikuu kote Ulaya.
Unaweza kufananisha hili na “jinsi watoto wa vigogo wanavyojibidiisha kujiunga na chuo cha diplomasia ili baadaye wapangiwe kazi huko.
Wakati huo huo, wizara za mambo ya nje zilianzishwa karibu katika mataifa yote ya Ulaya ili kuratibu balozi na wafanyakazi wao.
Maendeleo ya diplomasia yalizidi kuenea polepole hadi Ulaya ya Mashariki na hatimaye kufika Urusi mwanzoni mwa karne ya 18. Hata hivyo, mfumo wa diplomasia ulivurugwa sana na Mapinduzi ya Ufaransa kati ya mwaka 1789 na 1799 na miaka iliyofuata ya vita.
Mapinduzi yalipelekea watu wasiotoka katika familia au koo za watawala wakichukua nafasi za kdiplomasia za serikali ya Ufaransa, ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa kwa nafasi za wale waliotekwa na majeshi ya mapinduzi.
Vyeo vya awali vilifutwa. Mtawala aliyeibuliwa na vita hiyo, Napoleon Bonapatre pia alikataa kuheshimu kinga ya kidiplomasia (diplomatic immunity), akiwafunga wanadiplomasia kadhaa wa Uingereza wanaotuhumiwa kupanga njama dhidi ya Ufaransa (majasusi?)
Baada ya kuanguka kwa Napoleon, kongresi ya Vienna ya mwaka 1815 ilianzisha mfumo wa kimataifa wa vyeo vya kidiplomasia. Matumizi ya diplomasia katika kutatua migogoro kati ya nchi na nchi yaliendelezakwa karne hadi baada ya Vita vya Kidunia vya pili, ambapo chao balozi kikawa rasmi.
Diplomasia ya kisasa (modern diplomacy)
Kwa muda mrefu wa historia, diplomasia ilihusika na uhusiano wa nchi mbili, au mazungumzo kati ya mataifa mawili. Nchi au eneo husika mara nyingi lilikuwa na mikataba kadhaa ya biashara au mipaka, kila moja iliwekwa kwa nchi au eneo lingine. Mahusiano ya nchi na nchi nyingine ndio aina ya iliyozoeleka zaidi ya diplomasia.
Katika karne ya 20, diplomasia iliongezeka. Tangu wakati huo, Umoja wa Mataifa (UN), shirika la kimataifa linalofanya kazi ya kukuza ushirikiano na kutatua migogoro kati ya mataifa, limekuwa na jukumu kubwa katika diplomasia. Baraza Kuu, chombo kikuu cha Umoja wa Mataifa, kina wanachama 193 huku Palestina na Vatikani zikiwa “wanachama watazamaji.”
Diplomasia pia ilikua ikijumuisha mikutano mbalimbali ya kimatifa. Mikutano hiyo ni pamoja na mikutano kati ya viongozi wakuu wa serikali. Wakati mikutano hiyo huhusisha watu muhimu kutoka sekta mbalimbali kama vile uchumi ambapo viongozi wa biashara, mawaziri wa fedha/biashara na watu wengine muhimu huhudhuria.
Jinsi Diplomasia Inavyofanya Kazi
Diplomasia inakamilishwa kwa mazungumzo, au kujadiliana. Kwa kawaida, kila kundi katika mazungumzo litaomba zaidi ya wanavyotarajia kupata. Kisha wanaafikiana, au kuacha baadhi ya wanachotaka, ili kufikia makubaliano. Mara nyingi, mwanadiplomasia wa nje atasaidia na mazungumzo.
Wakati mwingine, upande mmoja katika mazungumzo hukataa maelewano. Hili linapotokea, wengine wanaohusika katika mazungumzo wanaweza kutumia vikwazo vya kidiplomasia. Vikwazo vya kidiplomasia vinahusisha kupunguza au kuondolewa kwa wafanyakazi wote wa ubalozi kutoka nchi iliyokosa.
Vikwazo vyepesi vya kidiplomasia vinaweza kuhusisha kukataa kwa rais kuzuru nchi iliyokosea au kukutana na viongozi wake.
Nchi zinaweza pia kutishia kutumia vikwazo vya kiuchumi, au adhabu. Kwa mfano nchi nyingi duniani zimeziwekea vikwazo Iran na Korea Kaskazini katika jithada za kuzuia nchi hizo kufanya majaribio ya silaha za nyuklia kinyume cha sheria.
Nyakati nyingine, wanadiplomasia wanatishia kutumia nguvu ikiwa suluhu haitafikiwa. Mnamo 1990, Iraki ilivamia nchi jirani ya Kuwait. Wakati Iraki ilipokataa kuondoka Kuwait, Umoja wa Mataifa uliidhinisha ufumbuzi wa kijeshi. Muungano, au kundi la mataifa yanayofanya kazi pamoja, ulipigana na jeshi la Iraki, na kuwalazimisha kutoka Kuwait.
Mazungumzo yenye mafanikio husababisha makubaliano ya kidiplomasia. Aina rasmi zaidi ya makubaliano ni mkataba, mkataba wa maandishi kati ya nchi.
Kwa mfano, Mkataba wa Versailles wa mwaka 1919 ulikomesha rasmi Vita vya Kwanza vya Dunia. Ulitiwa saini huko Versailles, Ufaransa.
Mikataba mingine inahitaji miaka mingi ya mazungumzo ya kidiplomasia.
Aina nyingine ya makubaliano ni mkataba, ambao hutiwa saini na mataifa mengi na kuwa sheria ya kimataifa. Maarufu zaidi ni Mikataba ya Geneva, ambayo inaelezea matibabu ya wafungwa wa vita, raia, na wafanyikazi wa matibabu katika eneo la vita. Mkataba wa kwanza ulitiwa sahihi huko Geneva, Uswisi, mwaka wa 1864. Mkataba wa nne, na labda muhimu zaidi, ulitiwa sahihi katika 1949 baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Itifaki, utaratibu usio rasmi wa kidiplomasia, hubadilisha au kupanua makubaliano yaliyopo. Kwa mfano, Itifaki ya Kyoto ulioafikiwa mwaka 1997 na kuanza kufanya kazi mwaka 2005 ni sasisho la Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 1994.
Kinga ya kidiplomasia
Kinga ya kidiplomasia ni aina ya ulinzi wa kisheria unaotolewa kwa wanadiplomasia ili kuwaruhusu kuepuka nguvu ya sheria katika nchi wanakofanya kazi.
Kinga ya kidiplomasia inatawaliwa na mkataba wa kimataifa uliotiwa saini mwaka wa 1960 unaoitwa Mkataba wa Vienna wa Mahusiano ya Kidiplomasia.
Mtu mwenye kinga ya kidiplomasia anaweza kuepuka uchunguzi wa polisi au kufunguliwa mashitaka ikiwa ameenda uhalifu, au anaweza kuepuka haja ya kujitetea katika kesi ya madai.
Ili nchi mwenyeji iweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu mwenye kinga ya kidiplomasia, inabidi kwanza nchi yake nchi ya asili imwondolee kinga kwanza.
Mkataba wa Vienna unawataka wanadiplomasia kuheshimu sheria za nchi mwenyeji. Jinsi gani mkataba huo utaheshimiwa inategemea pia mahusiano kati ya nchi husika.
Kinga inaweza kutumika kwa waume au wake za wanadiplomasia na wanafamilia wengine.
Uamuzi wa nani ana na nani hana kinga unabakia kwa nchi ambayo ilimtuma mwanadiplomasia husika. Sio juu ya mwanadiplomasia binafsi kudai.
Ikiwa mwanadiplomasia aliye na kinga amefanya uhalifu, hawezi kushtakiwa huko ugenini, lakini anaweza kufukuzwa katika nchi mwenyeji.
Uwezekano kwamba serikali itadai kinga kwa mmoja wa wanadiplomasia wake, au wanafamilia wao, hutegemea mambo kadhaa.
Ya muhimu zaidi ni jinsi mwanadiplomasia alivyo mkuu, na hii inaweza pia kutegemea jinsi jukumu lao lilivyo nyeti - kwa mfano, akiwa jasusi.
Kwa ujumla ni kwamba kinga hutegemea umuhimu wa kazi ya mtu husika kwa serikali yake. Ikiwa mhusika ni mtu anayefanya kazi kwa kiwango cha juu sana cha shughuli za serikali nje ya nchi, ubalozini, au ni jasusikwa ujumla, basi kiwango cha kinga ya kidiplomasia ni kamili kabisa na hakuna suala mjadala.
Mifuko ya kidiplomasia (diplomatic bag)
Mifuko ya kidiplomasia (“diplomatic bag” almaaruf “dip”) ni kifurushi chochote kilichotambulishwa na kufungwa ipasavyo, pochi, bahasha, begi, au chombo kingine chochote ambacho kinatumika kusafirisha barua rasmi, hati na vipengele vingine vinavyokusudiwa kutumika rasmi kwa mawasiliano kati ya Balozi/ubalozi/maafisa ubalozi na sehemu nyingine maalum (kwa mfano serikali ya nchi yao).
Kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna wa Mahusiano ya Kidiplomasia (VCDR), mifuko ya kidiplomasia "haitafunguliwa au kuzuiliwa” na mamlaka yoyote isipokuwa iliyolengwa na mtumaji.
Sheria ya kimataifa haiweki ukomo wowote kwa ukubwa unaoruhusiwa, uzito, au wingi wa mifuko ya kidiplomasia. Hata hivyo sheria hizo zinataka mifuko hiyo iwe na alama maaluma kuonyesha kuwa ni mifuko ya kidiplomasia.
Mara nyingi mifuko ya kidiplomasia hukabidhiwa kwa rubani au shirika la ndege ambao hubeba dhamana kuhakikisha kifurushi husika kinafika salama.
Uhusiano katika ya diplomasia na ujasusi
Takriban kila kilichoandikwa hapo juu kinahusiana kwa karibu na ujasusi. Hata hivyo kutokana na jukwaa hili la Substack linalotumika kuchapisha makala hizi kuwa na ukomo katika urefu wa makala husika, ni vema makala hii inaishia hapa kwa ahadi kuwa makala ijayo itajikita kwenye upande wa pili wa jinsi ujasusi unavyotumika kama nyenzo ya diplomasia.