Kifahamu kikosi cha Idara ya Usalama wa Taifa Tanzania kinachohusika na ulinzi wa viongozi (PSU)
Kitu cha kwanza kumfanya Jasusi atamani kuwa afisa wa Idara ya Usalama wa Taifa ni kusomewa kitabu kimoja cha James Bond. Kusomewa kwa sababu wakati huo Jasusi alikuwa mdogo tu, na alikuwa hafahamu lugha ya Kiingereza iliyotumuka kwenye kitabu hicho.
Miaka kadhaa baadaye, Jasusi alikumbana na mfululizi wa vitabu vya mwana-riwaya ya kijasusi, Marehemu Elvis Musiba, ambaye vitabu vyake bora kabisa katika fani hiyo vilimhusu jasusi wa kimataifa, Willy Gamba.
Lakini tukio lililompa hamasa zaidi Jasusi kutamani kazi hiyo ni pale alipokuwa mwanafunzi wa sekondari ya wavulana ya Tabora (Tabora Boys’ High School), ambapo shule hiyo ilipata bahati ya kutembelewa na aliyekuwa Rais wa Zanzibar wakati huko, Dkt Salmin Amour Juma aka komandoo.
Shule hiyo - pamoja na ya wasichana Tabora Girls’ - zilikuwa pekee nchini Tanzania kuwa za mkondo wa kijeshi. Na sare zetu zilikuwa magwanda ya kijeshi.
Wakati huo Jasusi alikuwa kiranja mkuu, ambapo kutokana na shule hiyo kuwa ya mchepuo wa kijeshi, wadhifa wake ulifahamika kama “chifu” kifupi cha Student’s Chief Commander (yaani kamanda mkuu wa wanafunzi). Na gwanda lake lilikuwa na “mikasi” mabegani.
Kutokana na wadhifa huo, Jasusi alikuwa sehemu ya maandalizi ya ziara ya Dkt Salmin shuleni hapo. Na hiyo ndio ilikuwa mara yake ya kwanza maishani kukutana na maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Licha ya kukutana na Afisa Usalama wa Taifa wa Mkoa (RSO) pia alikutana na Afisa Usalama wa Taifa wa Wilaya (DSO), lakini msisimko mkubwa zaidi ulikuwa alipokutana na maafisa kutoka kikosi cha Idara ya Usalama wa Taifa kinachohusika na ulinzi wa viongozi, yaani PSU, ambao walifika shuleni hapo kama msafara wa awali, kwa lugha ya kiintelijensia “advance party.”
Na zama hizo ambapo “Idara ya Usalama wa Taifa ilikuwa Idara ya Usalama wa Taifa kweli,” hao walinzi walikuwa kama wale wanaoonekana kwenye filamu. Kwa upande mmoja walikuwa “wanatisha” lakini kwa upande mwingine walikuwa wanamfanya kila mtu aitamani kazi yao - mavazi yao, miwani zao nyeusi…kila kitu.
Na ziara hiyo ya Dkt Salmin sio tu iliwasha kiu mpya ya Jasusi kutamani kuingia kwenye Idara ya Usalama wa Taifa ila pia “kwa namna flani” iliwezesha miaka kadhaa baadaye kutimia kwa ndoto yake hiyo.
Lakini makala hii sio kuhusu Jasusi bali PSU - kikosi cha Idara ya Usalama wa Taifa kinachohusika na ulinzi wa viongozi.
Je maafisa wanaoingia kwenye kikosi hicho hupatikana vipi? Je wana mafunzo maalum kuhusu “ubodigadi”? Ni kweli wapo “fiti” kukabili tishio lolote lile dhidi ya kiongozi?
Tiririka na makala hii ambayo ni moja ya nyingi kwenye safu hii ya “Simulizi za Jasusi” ambayo pamoja na mada nyingine, inakuletea habari/simulizi/kozi zinazohusiana na taaluma ya intelijensia.