Mbinu za kijasusi unazoweza kuzitumia katika maisha ya kila siku: mbinu ya kwanza [maalum kwa vijana wa kiume singo 'wenye ulimi mzito'] - KUTONGOZA (ashakum si matusi 😊)
Huu ni mwanzo wa mfululizo wa makala zitakazokufahamisha mbinu mbalimbali za kijasusi/kishushushu/kiintelijensia unazoweza kuzitumia katika maisha yako ya kila siku.
Maana
Lakini kabla ya kuingia kwa undani, ni muhimu kueleza maana ya maneno hayo matatu, yaani ujasusi, ushushushu na intelijensia.
Neno kuu hapo ni intelijensia. Neno hili linatokana na neno la kiingereza “intelligence”. Maana inayofahamika zaidi kuhusu intelligence ni akili. Lakini katika muktadha wa usalama, intelligence ina maana ya jumla ya “usalama wa taifa”. Hata hivyo, usalama wa taifa kwa kiingereza ni “national security”. Kukuondolea mkanganyo, maana ya intelligence katika muktadha wa usalama wa taifa haijawahi kupata mwafaka, kwa maana kuna mjadala endelevu kuhusu maana inayokubaliwa ya neno hilo.
Hata hivyo, kwa minajili ya mfululizo wa makala hizi, intelijensia ni masuala yanayohusu usalama wa taifa.
Ushushushu ni neno mbadala (la mtaani) la intelijensia. Na afisa wa Idara za Usalama wa Taifa hufahamika kama shushushu (wingi: mashushushu).
Ujasusi kwa kiingereza ni espionage. Na anayefanya ujasusi huitwa jasusi, kwa kiingereza ni spy. Lakini kama ilivyo kwenye maana ya intelijensia, maana ya ujasusi haijawahi kuwa na mwafaka wa pamoja.
Katika maisha ya kawaida, ujasusi ni kuchunguza kitu kwa siri na pengine kutumia mbinu zinazoweza kuwa sio halali.
Kitaasisi/kitaalamu, ujasusi ni kitendo cha Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi moja kutafuta na/au kupata taarifa za kiintelijensia za nchi nyingine na/au za Idara ya Usalama wa Taifa wa nchi hiyo.
Kuna mfululizo wa makala kuhusu ujasusi, unaochapishwa kwenye kijarida hiki, unaweza kusoma na kupata uelewa zaidi kuhusu taaluma hiyo
Ujasusi/ushushushu/intelijensia sio kwa ajili ya “kitengo” pekee
Tofauti na dhana kwamba masuala ya ujasusi/ushushushu/ intelijensia ni kwa ajili ya Idara za Usalama wa Taifa pekee, ukweli ni kwamba mbinu mbalimbali za kijasusi/kishushushu/kiintelijensia zinaweza kutumiwa katika maisha ya kila siku na kuwa na ufanisi mkubwa.
[Kwa minajli ya kuondoa mkanganyiko, kuanzia hapa nitatumia zaidi neno ujasusi na kuweka kando ushushushu/intelijensia]
Tofauti ya msingi kati ya matumizi ya mbinu za kijasusi zinazotumiwa na “kitengo”, kwa mfano, na mbinu za kijasusi anazoweza kutumia mtu asiyehusiana na “kitengo”, ni muktadha. Mbinu za kijasusi zinazotumiwa na kitengo ni kwa ajili ya masuala ya nchi. Kwa upande mwingine, mbinu za kijasusi zinazotumiwa na mtu asiye wa kitengo ni kwa ajili yake binafsi.
Hata hivyo, ni muhimu kutambua mapema kwamba wakati watu wa kitengo wana mamlaka kisheria kufanya ujasusi, raia wa kawaida anaweza kujikuta anavunja sheria katika baadhi ya maeneo.
Kwa mfano, wakati kunasa mawasiliano ya simu kwa njia za siri - kijasusi wanaita bugging ni halali kisheria kwa watu wa kitengo, ni kosa la jinai kwa mtu binafsi.
Hapo kuna habari mbaya na njema. Habari mbaya ni hiyo kwamba baadhi ya vitendo vya kijasusi ni makosa ya jinai kwa mtu binafsi. Habari njema ni kwamba “sheria zimewekwa ili zivunjwe.”
Hapana, hauhamasishwi kuvunja sheria bali kuna nyakati unalazimika kuvunja sheria. Hata hao watu wa kitengo sio mara zote huwa wanapata ruhusa ya kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria. Na katika ujasusi nje ya nchi, asilimia kubwa ya matendo ni ya uvunjifu wa sheria.
La muhimu sio kuvunja sheria as such bali kwanini unavunja sheria husika. Kama ni kwa nia njema, well, just do it.
Kwenye udukuzi - mada ambayo utafundishwa katika mfululizo wa makala hizi - inafundishwa kwamba moja ya vitu viwili muhimu kwenye tasnia hiyo ni intent - yaani dhamira, kwa Kiswahili. Kama dhamira yako ni nzuri unapodukua akaunti ya mtu, basi angalau kuna “moral justification” (uhalali kiroho).