Mbinu za kijasusi unazoweza kuzitumia katika maisha ya kila siku: mbinu ya tatu - jinsi ya kugundua kama mwenza "anachepuka" [sehemu ya kwanza ]
Huu ni mwendelezo wa mfululizo wa makala zitakazokufahamisha mbinu mbalimbali za kijasusi/kishushushu/kiintelijensia unazoweza kuzitumia katika maisha yako ya kila siku.
Makala hii ni ya tatu katika mfululizo huu. Endapo hukubahatika kusoma makala mbili zilizopita, soma hapa
Katika makala hii utafundishwa mbinu mbalimbali za uhakika za kukusaidia aidha kujiridhisha kuwa mwenza wako ni mwaminifu katika mahusiano yenu au endapo unahisi kuwa “anachepuka” na unataka kuthibitisha.
Makala hii inatarajiwa kuwa ndefu na kuna uwezekano ikaendelea kwenye toleo lijalo au hata matoleo mawili zaidi. Urefu tarajiwa wa makala unatokana na ukweli kwamba mada husika sio tu ni nyeti bali ina “aspects” mbalimbali. Kwa mfano wakati kuna urahisi kwa mwenza wa kiume kumchunguza mwenza wa kike, hususan kutokana na jamii yetu kuwa ya mfumo dume, ni mtihani mkubwa kwa mwenza wa kike kumchumguza mwenza wa kiume.
Kadhalika, zoezi zina la aidha kujiridhisha au kuthibitisha uadilifu kwenye mahusiano linategemea aina ya mahusiano husika, kwa maana kama ni uhusiano kati ya boyfriend na girlfriend, au kati ya wachumba, au kati ya wanandoa.
Jingine la kuzingatiwa ni muda wa mahusiano husika, kwa mfano kama ni boyfriend na girlfriend, uhusiano una muda gani tangu uanze, na kama wanandoa, ndoa husika ina muda gani, na pia endapo kuna watoto ndani ya ndoa hiyo.
Jambo jingine la muhimu sana katika mbinu zitakazofundishwa ni ukweli kwamba baadhi sio tu zinaweza kuwa kinyume cha sheria bali pia zaweza kukuingiza matatizoni. Kwahiyo ni muhimu kujiridhisha kuwa endapo utaamua kutumia mbinu husika, unaelewa “risks” zinazoambatana na uamuzi huo.