#SimuliziZaJasusi: Makala hii inajibu swali ninaloulizwa takriban kila siku "ninataka kujiunga na Idara ya Usalama wa Taifa, je nifanyeje?"
Pamoja na maovu mengi yaliyofanywa na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) dhidi ya Jasusi ikiwa ni pamoja na majaribio kadhaa ya kumtoa uhai, bado anaweza kujipongeza bila shaka katika angalau vitu viwili chanya.
Cha kwanza, Jasusi amefanikiwa sana kutenganisha taaluma ya uafisa usalama wa taifa (ushushushu) vs hujuma zinazofanyiwa na Idara ya Usalama wa Taifa dhidi yake. Licha ya yote yanayofanywa dhidi yake, Jasusi ameendelea kuwa mmoja wa wadau wakuu na adimu wanaofundisha au kuhabarisha kuhusu mengi yanayohusiana na taaluma hiyo pasi kuathiri utendaji kazi wa TISS.
Sambamba na hilo, kitabu cha Jasusi kiitwacho “SHUSHUSHU” kimesaidia sana kuondoa baadhi ya dhana potofu dhidi ya Idara ya Usalama wa Taifa na taaluma ya intelijensia kwa ujumla.
Maelfu ya watu waliokisoma kitabu hiki bora kabisa wameweza kuelewa kuwa tofauti na dhana kuwa Idara za usalama wa taifa ni “taasisi za wauawaji” zinazotesa na kuua watu, ukweli ni kwamba taasisi hizo ni nyenzo muhimu kwa ustawi na uhai wa taifa lolote lile. Naam, Idara yetu ya Usalama wa Taifa ina sifa mbaya hasa kwa vile inatumika zaidi kwa maslahi binafsi kuliko maslahi ya taifa, lakini hiyo haiondoi umuhimu wa taasisi hiyo na nyinginezo za intelijensia duniani.
Sambamba na hayo, kwa miaka kadhaa, Jasusi amekuwa moja ya sauti adimu kabisa zinazopigania mageuzi katika Idara ya Usalama wa Taifa ili taasisi hiyo iwe na ufanisi zaidi. Angalia twiti hii ya Julai 2012, miaka 10 na ushee iliyopita.
Na pengine ni kutokana na mambo hayo mawili hapo juu, Jasusi amejikuta akiandamwa takriban kila siku na swali kutoka kwa Watanzania mbalimbali kuhusu jinsi gani wanaweza kujiunga na Idara ya Usalama wa Taifa.
Yayumkinika kuhisi kuwa jitihada zake zimesaidia sio tu kuondoa taswira hasi dhidi ya Idara ya Usalama wa Taifa bali pia zimeleta mvuto kwa Watanzania wengi tu kutamani kujiunga na taasisi hiyo.
Makala hii inajibu swali hilo lililomo kwenye kichwa cha habari cha makala hii “ninataka kujiunga na Idara ya Usalama wa Taifa, je nifanyeje?” Majibu ya swali hili yanaweza kuwa na msaada kwako pia hata kama hujawahi kumuuliza Jasusi swali hilo.