Tathmini ya kiintelijensia: Kauli za Dkt Nchimbi jana, Hotuba ya IGP Wambura na Tamko la Msemaji wa Polisi, na msimamo wa Chadema kuhusu maandamano Septemba 23 endapo Rais Samia hatotimiza matakwa yao
Utangulizi:
Majuzi, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mheshimiwa Freeman Mbowe aliongea na viongozi wa chama hicho pamoja na waandishi wa habari kuhusu kuuawa kwa kiongozi mwandamizi wa Chadema, marehemu Ali Mohamed Kibao, sambamba na suala zima la utekaji.
Pamoja na mambo mengine, Mheshimiwa Mbowe alitoa orodha ya matakwa ya chama hicho kwa Rais Samia Suluhu.
Matakwa hayo ni pamoja na
Kumtaka Rais Samia awalete maafisa wa Scotland Yard kuchunguza utekaji na mauaji nchini Tanzania, kwa sababu jeshi la polisi haliwezi kujichunguza kama watuhumiwa.
Rais Samia kuwafuta kazi Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni, IGP Camillus Wambura, DCI Kingai, na DGIS Selemani Mombo.
Kadhalika, Mheshimiwa Mbowe alitangaza kuanza kwa kampeni ya Samia Must Go, kwa mantiki kwamba Sheria ya Usalama wa Taifa iliyopitishwa hivi karibuni imemfanya Rais kuwa Mkuu halisi wa Idara ya Usalama wa Taifa, kwahiyo suala la watu kutekwa na kuuawa linaangukia mikononi mwake.
Vilevile, Mheshimiwa Mbowe alimpa Rais Samia hadi Septemba 21 kutimiza matakwa hayo ya Chadema, na asipofanya hivyo, chama hicho kitaanza maandamano Septemba 23.
TANGAZO
Juzi, IGP Wambura aliongea na viongozi wa jeshi la polisi ambapo pamoja na mambo mengine alieleza kuwa hali ya usalama nchini Tanzania ni shwari, kauli ambayo moja kwa moja ilikinzana na madai na matakwa ya Chadema.
IGP Camillus Wambura amesema hali ya usalama nchini ni shwari kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi ambapo amevipongeza vyombo vya ulizi na usalama kwa kuhakikisha nchi inakuwa na amani na utulivu na wananchi wanaendelea na shughuli zao.
Aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano mkuu wa Mwaka wa Maafisa wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro ambapo mgeni rasmi wa mkutano huo alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo.
Aidha, IGP. Wambura amesema jeshi la polisi limejiimarisha zaidi katika mikakati ya kuzuia uhalifu ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa kuwashughulikia waalifu, na kutoa rai kwa viongozi wa dini na familia kulea jamii kwa kufuata mila, desturi na misingi ya dini.
Kadhalika, jana, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, alieleza kuwa Jeshi hilo limepiga marufuku maandamano yaliyoandaliwa na CHADEMA, ambayo yalikuwa yamepangwa kufanyika Septemba 23 katika jiji kuu la kibiashara, Dar es Salaam. Marufuku hiyo imetolewa kwa lengo la kudumisha amani na usalama wa wananchi.
Misime aliongeza kwamba hatua hii imechukuliwa kwa sababu baadhi ya viongozi na wafuasi wa CHADEMA wamekuwa wakipanga mikakati ya kuchochea vurugu nchini, hali ambayo inaleta hatari kwa amani ya nchi. Alisema kuwa mara kadhaa serikali imeagiza kufanyika kwa uchunguzi ili kubaini walipo wanachama waliodaiwa kupotea, lakini baadhi ya watu wanaendelea kutoa mipango inayolenga kuharibu amani.
"Kwanini wanataka kututoa kwenye reli hatua za kiupelelezi zinazoendelea baada ya Rais Samia Suluhu kuagiza kufanyika kwa uchunguzi, mara kadhaa viongozi na wafuasi wamekuwa wakipanga na kuratibu mikakati mbalimbali na kutoa mipango yenye lengo la leta vurugu nchini ili kuharibu amani ya nchi yetu kwasababu zao wenyewe, kutokana na taarifa hiyo jeshi la polisi nchini limepiga marufuku kuacha kuendelea kuhamasisha kujihusisha katika uhalifu huo" alisema Misime.
Lakini pengine kubwa zaidi ni kauli ya jana ya Katibu Mkuu wa CCM, Dokta Emmanuel Nchimbi ambapo pamoja na mambo mengine alieleza bayana kuwa tuhuma kwamba Mheshimiwa Mbowe na Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika kuhusika na mauaji ya marehemu Kibao hayana ukweli.
Kadhalika, Dkt Nchimbi alidai kwamba kuna jitihada za kulichonganisha Jeshi la Polisi na wananchi akidai kuwa jeshi hilo halihusiki na utekaji.
Vilevile, alisema kwamba kampeni ya Samia Must Go haiwezekani kama ambavyo kampeni za awali za kutaka Mheshimiwa Mbowe aachie ngazi hazikufanikiwa.