Uchambuzi wa kiintelijensia: kauli za Mbowe kuhusu maridhiano na CCM, wanaomdhihaki kuwa 'amelamba asali'
Muhtasari: ripoti hii ya kiintelijensia inaeleza na kutathmini kauli mbili za Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mheshimiwa Freeman Mbowe, ambapo alisikika akieleza msimamo wake kuhusu majadiliano yanayoendelea katika ya chama chake na CCM kuhusu “maridhiano”, sambamba na kusikitishwa kwake na wanaomdhihaki kuwa “amelamba asali” .
Katika uchambuzi unaojenga ripoti hii, kauli hizo za Mheshimiwa Mbowe zitachambuliwa kwa tafsiri pana, ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini endapo misimamo aliyoiweka hadharani - ambapo angalau mara moja amemtaja Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mheshimiwa Tundu Lissu - inaimarisha au kuathiriwa nafasi yake kama mwanasiasa mwenye nguvu kuliko wote ndani ya chama hicho; mkinzano wa waziwazi katika ya kauli zake na za Katibu Mkuu wa chama hicho Mheshimiwa John Mnyika; faida au athari kwa Chadema; na mustakabali wa siasa za Tanzania kwa kuhusisha msimamo wa Mheshimiwa Mbowe na Chadema kwa ujumla.
Mbinu husika: uchambuzi wa kiintelijensia uliomo kwenye ripoti hii umetumia mbinu ya Uchambuzi wa Nadharia Zinazoshindana (Analysis of Competing Hypotheses kwa kifupi ACH). Mbinu hii ambayo ni maarufu zaidi katika chambuzi za kiintelijensia, huwa na ufanisi zaidi pale ambapo tayari kuna nadharia kuhusu tukio husika.