Uchambuzi wa kiintelijensia kuhusiana na ajali ya helikopta iliyopelekea kifo cha Mkuu wa Majeshi ya Kenya, Jenerali Francis Ogolla jana, ajali kweli au 'kuna mkono wa mtu'?
Mkuu wa Majeshi ya Kenya, Jenerali Francis Ogolla alifariki jana alasiri baada ya helikopta ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kuanguka eneo la Sindar, Kaunti ya Elgeyo-Marakwet.
Taarifa ya kifo chake ilithibitishwa na Rais William Ruto katika hotuba yake kwa taifa hilo la Afrika Mashariki.
Leo saa 2:20 usiku, taifa letu lilipata ajali mbaya ya angani katika eneo la Sindar, lokesheni ya Kaben, tarafa ya Tot, kaunti ya Elgeyo Marakwet. Nina masikitiko makubwa kutangaza kuaga kwa Jenerali Francis Omondi Ogolla, Mkuu wa Majeshi ya Kenya.
William Ruto - Rais wa Kenya
Pamoja na Jenerali Ogolla, helikopta husika ilikuwa na maafisa wengine 11 wa jeshi la Kenya (KDF), ambapo wawili kati yao walinusurika.
Maafisa waliofariki ni Brigedia Swale Saidi, Kanali Duncan Keittany, Luteni Kanali David Sawe, Meja George Benson Magondu, Kapteni Sora Mohamed, Kapteni Hillary Litali, Sajenti Kiongozi John Kinyua Mureithi, Sajenti Cliphonce Omondi, na Sajenti Rose Nyawira.
Wasifu wa Jenerali Ogolla
Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Kenya, Jenerali Francis Ogolla aliyezaliwa mwaka 1962 huko Kisumu, Kenya, alijiunga na chuo ch kijeshi mwaka 1981 na kuanza kutumikia Jeshi la Ulinzi la Kenya mwaka 1984.
Alitawazwa kama Luteni wa Pili tarehe 6 Mei 1985 na akapelekwa kwa Jeshi la Anga la Kenya (KAF). Alipata mafunzo ya urubani na baadaye kuwa rubani mkufunzi katika Jeshi hilo la Anga.
Pia alipata mafunzo katika nyanja zingine zikiwemo ujasusi wa picha, kukabiliana na ugaidi na uchunguzi wa ajali.
Jenerali Ogolla alikuwa mhitimu wa chuo cha kijeshi cha ÉcoleMilitaire de Paris cha Ufaransa na Chuo cha Kitaifa cha Ulinzi cha Kenya. Alikuwa na Diploma katika Masomo ya Kimataifa na Sayansi ya Kijeshi kutoka Chuo Kikuu cha Egerton, Kenya, na Shahada ya Sanaa katika Sayansi ya Siasa, Migogoro ya Silaha na Mafunzo ya Amani. Pia alikuwa na Shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Stadi za Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.
Jenerali Francis Ogolla alipanda ngazi hadi kuwa Meja Jenerali na kuteuliwa kuwa Kamanda wa Jeshi la Anga la Kenya mnamo Julai 2018.
Hapo awali aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Mafunzo, Kamandi na Wafanyakazi ikiwa ni pamoja na Naibu Kamanda wa Jeshi la Anga la Kenya, Kamanda wa Kambi ya Jeshi la Anga ya Laikipia, Afisa Mkuu wa Mafunzo ya Ndege za kivita, Mwalimu Mkuu wa Usafiri wa Ndege katika Shule ya Mafunzo ya Urubani kwa Jeshi la Anga na Afisa wa Dawati la Operesheni katika Jeshi la Anga.
Pia alihudumu katika iliyokuwa Yugoslavia kama Mwangalizi na Afisa Habari wa Kijeshi kutoka 1992 hadi 1993, kama mwenyekiti wa Ushirika wa Kijeshi wa Kikristo kutoka 1994 hadi 2004 na Mwenyekiti mwenza wa Chama cha Wakuu wa Majeshi ya Anga ya Afrika kati ya 2018 na 2019.
Mnamo Aprili 28, 2023, Jenerali Francis Ogolla alipandishwa cheo kutoka cheo cha Luteni hadi cheo cha Jenerali na kuteuliwa na kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) na Rais Ruto. Kabla ya uteuzi huo Jenerali Ogolla alikuwa Makamu Mkuu wa Majeshi ya Kenya.
Jenerali Ogolla ameacha mke aitwaye Aileen, na watoto wawili na mjukuu. Inaelezwa kuwa pamoja na kupenda kujisomea, alipenda pia mchezo wa gofu.