Uchambuzi wa kiintelijensia kuhusu kukamatwa Mbowe, Lissu, Mnyika na mamia ya wafuasi wa Chadema
Jana, kwa mara ya kwanza tangu Rais Samia Suluhu aingie madarakani Machi 2021, viongozi wote wakuu wa Chadema - Mwenyekiti Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu na Katibu Mkuu John Mnyika - walikamatwa na jeshi la polisi katika kile kilichoelezwa kama kuzuwia mkusanyiko wa chama hicho kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani uliopangwa kufanyika mkoani Mbeya.
TANGAZO
Walio nje ya Tanzania wanaweza kununua vitabu hivi HAPA
Uchambuzi huu wa kiintelijensia unaonyesha athari na kukamatwa huko hususan kwenye falsafa ya 4Rs ya Rais Samia, chaguzi muhimu zijazo - uchaguzi wa serikali za vitongoji, vijini na mitaa hapo Novemba na uchaguzi mkuu Oktoba mwakani - pamoja na hali ya kisiasa kwa ujumla nchini Tanzania.
Kilichojiri
Kukamatwa huko kulifanyika katika jiji la Mbeya ambako Chadema ilikuwa imepanga kufanya mkutano wa hadhara kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana.
Jeshi la Polisi lilipiga marufuku tukio hilo, wakidai kuwa lililenga kuchochea vurugu. Licha ya marufuku hiyo, viongozi na wafuasi wa Chadema walikusanyika, na kusababisha kukamatwa kwa watu wengi. Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na viongozi mashuhuri kama Mbowe, Lissu, na John Mnyika, ambao ni viongozi wakuu wa chama hicho kitaifa, pamoja na takriban wafuasi 400.