Uchambuzi wa Kiintelijensia Kuhusu Mabadiliko ya Baraza La Mawaziri Yaliyofanywa na Mama Samia Jana 08.01.22
Hatimaye jana Januari 8, Mama Samia Suluhu alitangaza mabadiliko ya baraza lake la mawaziri ambayo jasusi wako alieleza kuwa yangetokea, kabla ya Mama Samia mwenyewe kuthibitisha.
Kadhalika, jasusi alifanya uchambuzi mfupi wa kiintelijensia katika blogu ya Ujasusi (ya lugha ya Kiingereza) kuhusu mabadiliko hayo
Katika mabadiliko hayo, Mama Samia amemrejesha Nape Nnauye katika nafasi ileile aliyotimuliwa na Rais Magufuli, ya Uwaziri wa Habari, (ambayo sasa ina inahusu pia Mawasiliano na Teknolojia ya Habari). Magufuli alimfukuza kazi Nape kwa “kosa” la kutimiza wajibu wake kama Waziri husika kufuatilia kitendo cha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuvamia kituo cha habari cha Clouds, jijini Dar es Salaam.
Mwingine aliyeteuliwa ni Pindi Chana, kada wa muda mrefu wa CCM, ambaye naye alikuwa mhanga wa Magufuli aliyemuondoa kwenye nafasi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya katika mazingira ya kutatanisha. Ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)
Mawaziri wengine wapya ambao wamepandishwa vyeo kutoka unaibu waziri ni Hamad Yusuph Masauni, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, na Dkt Angelina Mabula, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na Hussein Bashe aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo.
Kabla ya uteuzi huo, Masauni alikuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Mabula na Bashe walikuwa manaibu katika wizara hizo hizo.
Walioteuliwa unaibu waziri ni Ridhiwani Kikwete, Mbunge wa Chalinze ambaye pia ni mtoto wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete; Anthony Mavunde; Jumanne A. Sagini; Dkt Lemomo Ole Kiruswa; na Atupele Fredy Mwakibete.
Ridhiwani anakuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mavunde anakuwa Naibu Waziri wa Kilimo; Sagini anakuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani; Dkt Kiruswa anakuwa Naibu Waziri wa Madini; na Mwakibete anakuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi).
Uchambuzi huu wa kiintelijensia kuhusu mabadiliko hayo unatoa tafsiri pana kwa kuangalia wateuliwa na “sababu za kuteuliwa wao,” mapokeo “huko mtaani” sambamba na kueleza sababu za “kutoswa” kwa Mawaziri Profesa Palamagamba Kabudi, Profesa Kitila Mkumbo, William Lukuvi, Geofrey Mwambe, na Naibu Waziri Mwita Waitara.