Uchambuzi wa kiintelijensia kuhusu Rais Samia kumtumbua Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Saidi Masoro, na kumteua Balozi Ali Siwa kushika wadhifa huo
Jana kwa mara ya pili, Rais Samia Suluhu alimtumbua Mkurugenzi Mkuu mwingine wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Safari hii ilikuwa zamu ya Saidi Masoro ambaye aliteuliwa na Rais Samia kushika wadhifa huo Januari 3, 2023. Kwahiyo, Masoro amedumu katika nafasi hiyo kwa miezi minane hivi, muda unaoingia kwenye historia kama Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa aliyedumu kwa muda mfupi kabisa.
Masoro nae aliteuliwa kufuatia kutumbuliwa kwa mtangulizi wake, Diwani Athumani, ambaye “kwa hasira”, alisusa uteuzi aliopewa na Rais Samia kuwa Katibu Mkuu Ikulu, na kupelekea Mkuu huyo wa nchi kulazimika kutengua uteuzi huo mpya wa Diwani.
Aliyeteuliwa kushika nafasi ya Masoro ni Balozi Ali Siwa, Mkurugenzi wa zamani wa Operesheni za Ndani (DOI) katika Idara ya Usalama wa Taifa, kabla ya kushika nafasi mbalimbali za kidiplomasia.
Uchambuzi huu wa kiintelijensia unajikita katika kueleza kwanini Masoro ametumbuliwa, na pia kumtathmini Balozi Siwa sio tu kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo nyeti bali pia wakati huu ambapo serikali ya Rais Samia inakabiliwa na changamoto kadhaa.