Urais Marekani: Nani Kuibuka Mshindi Kati ya Kamala na Trump Leo?
Watu kadhaa wamemuomba Jasusi afanye uchambuzi kuhusu kinyang’anyiro cha kuwania urais wa Marekani ambapo wagombea Kamala Harris wa chama cha Democrats na Donald Trump wa chama cha Republican wanachuana vikali.
Uchaguzi huo unafanyika kesho Novemba 5 unatajwa kama miongoni mwa chaguzi ambao wagombea wamekabana koo kweli kweli ambapo hadi leo, masaa machache tu kabla ya siku ya uchaguzi, hakuna mgombea kati ya Kamala na Trump ambaye kura za maoni zinamwonyesha akimwacha mwenzie mbali.
Kura za maoni zinasemaje?
Kama ilivyoelezwa hapo juu, kura mbalimbali za maoni zinaonyesha kuwa Kamala na Trump wanakabana koo kwelikweli, yaani tofauti kati yao ni kile wanaita “sare kitakwimu”.
Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, kura za maoni - njia kuu ya kubashiri matokeo ya uchaguzi - zimekuwa hazimianiki sana. Mfano mzuri ni katika kinyang’anyiro cha urais wa Marekani mwaka 2016 ambapo hadi siku ya uchaguzi, kura za maoni zilikuwa zikionyesha kuwa mgombea wa Democrats wakati huo, Hillary Clinton, alikuwa amemzidi mgombea wa Republican, Trump, kwa asilimia za kutosha. Lakini mwishowe Trump akambwaga Hillary.
Bradley Effect
Kuna kitu kwenye chaguzi za Marekani kinachoitwa Bradley Effect. Bila haja ya kuingia kiundani kuhusu asili ya kitu hicho, maana yake ni kwamba mara nyingi kunapokuwa mgombea Mweusi (Black), watu weupe (Whites) wanaotoa maoni kwenye kura za maoni wanaficha ukweli wa dhamira yao ya kura ili wasionekane wabaguzi wa rangi.
Kwahiyo inawezekana baadhi ya watu weupe wanaohojiwa kwenye kura za maoni, hawasemi ukweli kuhusu Kamala - ambaye sio Mweupe - ili wasionekane wabaguzi wa rangi.
Uchaguzi wa akili mnemba
Moja ya mambo yaliyotawala kwenye uchaguzi huu ni matumizi ya akili mnemba hasa kwa lengo la kupotosha. Na jitihada za matumizi ya akili mnemba kwenye kampeni yalifanywa zaidi na wafuasi wa Trump, huku kukiwana uthibitisho kwamba baadhi ya “taarifa” zilizowekwa mtandaoni zilitengenezwa Urusi.
Kwa vile Jasusi amekuwa akifuatilia kwa karibu kampeni za uchaguzi huo, na kushuhudia”mabalaa ya akili mnemba” ndio maana awali alishawishika kuandaa kozi ya siku 30 ya mada hiyo, kwa sababu licha ya umuhimu wa akili mnemba, kuna upande wa pili wa hatari mno. Kwa bahati mbaya alijitokeza mtu mmoja tu kujisajili kwa ajili ya kozi hiyo 😢
Endapo Kamala atashindwa, basi mongoni mwa vitu vitakavyokuwa vimechangia ni pamoja na matumizi ya akili mnemba kwenye kampeni dhidi yake.
Kabla ya kubashiri nani atashinda, hali itakuwaje baada ya uchaguzi?
Endapo Kamala atashindwa, yayumkinika kuamini atakubali matokeo na safari yake itakuwa imeishia hapo.
Lakini endapo Trump atashindwa, PATACHIMBIKA. Kama ambavyo hakukubali matokeo ya uchaguzi wa 2020, ndivyo inavyotarajiwa kwamba hatokubali matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu endapo atashindwa. Na ameshawaandaa wafuasi wake kisaikolojia kwamba endapo hatoshinda, kamwe wasiyatambue matokeo ya uchaguzi huo.
Nani atashinda kati ya Kamala na Trump?
Msaada Tutani kutoka kwa akili mnemba
Japo tayari Jasusi alishakuwa na ubashiri wake nafsini, juzi aliona hakuna ubaya akiwasikiliza “rafiki zake wapya” yaani modeli mbalimbali za akili mnemba. Aliwahoji “rafiki zake” 10, kama inavyoonekana pichani.